DK. SLAA AIBUKA NA FARU

Na Mwandishi Wetu, Mikumi KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbrod Slaa, ameibuka na kusema anazo nyara... thumbnail 1 summary

Na Mwandishi Wetu, Mikumi KATIBU Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk. Willbrod Slaa, ameibuka na kusema anazo nyaraka za siri, kuhusu mauaji ya faru yaliyofanyika hivi karibuni katika Hifadhi ya Serengeti, mkoani Mara.

Dk. Slaa, alisema nyaraka alizonazo zinaonyesha kuna mtandao mkubwa wa ujangili, unaohusisha vigogo wakubwa serikalini, watumishi wa vyombo vya dola, askari polisi na watumishi wa Idara ya Usalama wa Taifa.

Dk. Slaa alitoa kauli hiyo juzi, wakati akiwahutubia mamia ya wananchi wa vijiji vya Kata ya Malinyi, Mikumi na Ruaha.

Alisema nyaraka hizo, zinaelezea kiundani suala zima la mtandao wa ujangili.

Alisema mauaji ya wanyama adhimu faru, yaliyofanyika katika Mbuga ya Serengeti, ni dalili ya hujuma kubwa katika sekta ya maliasili ambazo zinafanywa na mtandao huo.

Alisema kumekuwapo na tabia ya kuwanyamazisha wabunge wanaotaka kupanua mjadala wa ufisadi mkubwa unaoendelea kuteketeza maliasili za nchi, wakiwamo twiga na faru.

“Naliomba Bunge kuacha kuminya mijadala, inayolenga kuibua matatizo ambayo tunaweza kuyatafutia tiba katika sekta mbalimbali za uchumi na maendeleo ya nchi… ninashangazwa kuona Serikali inaendelea kufumbia macho mtandao huo.

“Watanzania wenzagu wa Ulanga, hii ndiyo hali halisi namna ambavyo Serikali ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), imetufikisha hapa tulipo leo, ufisadi umetamalaki kila mahali, leo hapa ninazo mkononi kwangu nyaraka za siri zinazoelezea namna ambavyo faru wetu, wale wanyama adimu walivyouawa hivi karibuni huko Serengeti.

“Kwa mwananchi wa kawaida, inaweza kuwa vigumu kuelewa haraka umuhimu wa faru katika masuala ya uchumi.

“Kwa wale wanaofuatilia Bunge, watakuwa wameona juzi Mbunge wa Iringa Mjini, Mchungaji Peter Msigwa (Chadema), alivyoambiwa bungeni baada ya kuibua suala hili la kuuawa kwa faru…mimi sitaki kuingia huko kwenye kamati yao na kile wanachofanya.

“Lakini nyaraka nilizonazo hapa zinaeleza bayana namna ambavyo faru hao waliuawa, huku wahusika, wakiwemo askari polisi majina wametajwa hapa, maliasili zetu wakiwemo wanyama, ziko hatarini kumalizwa kutokana na uzembe wa serikali kulea ufisadi.

“Kama Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki anaona kuna mahali angeweza kuchukua hatua, lakini anashindwa kwa sababu kuna watu wengine wanapaswa kuchukua hatua zaidi,” alisema.

Pamoja na mambo mengi, ameiomba Serikali kuwachukulia hatua kali wale wanaothibitika kufanya vitendo vya ubadhirifu wa mali za umma.

Chanzo: Mtanzania