MSIGWA: WALIOFUKUZWA MALIASILI NI VIDAGAA

na Danson Kaijage, Dodoma MSEMAJI Mkuu wa kambi ya upinzani bungeni, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA) amesema watumishi watatu wa Wizar... thumbnail 1 summary

na Danson Kaijage, Dodoma MSEMAJI Mkuu wa kambi ya upinzani bungeni, Mchungaji Peter Msigwa (CHADEMA) amesema watumishi watatu wa Wizara ya Maliasili waliofukuzwa kazi kwa kashfa ya utoroshaji wa wanyamapori hai nje ya nchi ni vidagaa, kwani wahusika wakubwa wameachwa.
Alisema katika suala hilo kuna mtandao mkubwa, na kwamba watumishi hao waliofukuzwa kazi, wametolewa kafara.
Juzi, Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamisi Kagasheki alitangaza kuwafukuza kazi Mkurugenzi wa Wanyamapori, Obeid Mbangwa ambaye wakati kashfa hiyo inatokea alikuwa Mkurugenzi Msaidizi Matumizi ya Wanyamapori, Simon Charles Gwera na Frank Mrema, waliokuwa maofisa Uwindaji wa Kitalii Cites na utalii na picha (Arusha).
Akizungumza na waandishi wa habari mjini hapa jana, Mchungaji Msigwa ambaye pia ni waziri kivuli wa wizara hiyo, alisema ili kuvunja mtandao huo, kunahitajika ushirikiano na kwamba kutokana na ubabe wa waziri Kagasheki suala hilo linaweza lisifanikiwe.
“Asijisifu kwa kuwafukuza maofisa hao, akumbuke Mwalimu Julius Nyerere alisema serikali inayokimbizana na watu wadogo ni dhaifu na sio suluhisho la matatizo.
“Waliofukuzwa kazi ni vidagaa, big fish wameachwa… na katika suala hili kuna mtandao mkubwa ambao unahitaji ushirikiano wa wadau mbalimbali wakiwamo wabunge kuuvunja,” alisema.
Aidha, alisema kitendo cha kutangaza kuwafukuza kazi maofisa hao si juhudi zake bali ni za aliyekuwa waziri wa wizara hiyo, Ezekiel Maige.
Pamoja na mambo mengine, alisema kuwa ndege ya Qatar inayodaiwa kutorosha wanyapori hao ni ya kijeshi na kuhoji iliingiaje nchini na watu waliohusika wamechukuliwa hatua gani.
“Kuna watu walikuwa wakifungua geti ili ndege hiyo ipite, mbona hawajachukuliwa hatua? Anataka umaarufu, wakati tembo na faru wanaendelea kuisha,” alisema.
“Lakini jambo jingine ambalo nataka kuwaambia Watanzania ni kuwa kitendo cha kuwakemea watumishi wa wizara kutokutoa taarifa ni dalili za kutaka kuendelea kukumbatia ufisadi.”
Alisema kitendo hicho pia ni kulihujumu Bunge na kwamba ufisadi wa Richmond uliibuliwa kwa njia hiyo, hivyo kwa kauli yake hiyo anaonekana anatetea ufisadi.
Hata hivyo, alisema Balozi Kagasheki anatakiwa awajibike kama alivyowajibika aliyekuwa Waziri wa Wizara hiyo, Ezekiel Maige, kwani alishindwa kushughulikia masuala ya vitalu.
Pamoja na hilo, alikanusha kuwa na uhusiano wa karibu na makampuni ya uwindaji pamoja na wafanyabiashara hao na kusema akitokea mtu mwenye ushahidi wa hilo, atakuwa tayari kujiuzulu ubunge.
Pia alisema waziri huyo anaongoza wizara hiyo kwa ubabe na kujitafutia umaarufu kwa utendaji wa waziri aliyemtangulia na kuongeza kuwa wizara hiyo haihitaji ubabe, bali ushirikiano na wadau mbalimbali.
Wakati huohuo, alisema kuwa waziri huyo hana uadilifu kwani alipokuwa akifanya kazi katika kampuni ya Weap, alihojiwa kutokana na akaunti yake kuingizwa dola 270,000 na kuhoji fedha hizo zilikuwa kwa ajili ya biashara gani.
Kuhusu maoni ya kambi hiyo, alisema waziri huyo ameonesha udhaifu katika kujibu hoja, na badala yake kujikita katika propaganda kwa makosa ya uchapaji.
“Katika hotuba yangu tulikosea, tulimtaja Lazaro kuwa Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Karatu, lakini ukweli ni kuwa Japhet Lazaro ni Mwenyekiti wa Kitongoji wa CCM Karatu ambaye anajihusisha na ujangili, sasa badala ya kujibu hoja amenishambulia mtoa hoja na kuhoji uchungaji wangu,” alisema.
Chanzo: Tanzania Daima