UTATA WATANDA KWA WAKAZI SERENGETI

na Asha Bani UTATA umetanda kwa wafugaji wa Kimaasai eneo la Serengeti kutokana na kuzagaa taarifa kwenye mitandano ya kimataifa kuwa, ... thumbnail 1 summary


na Asha Bani
UTATA umetanda kwa wafugaji wa Kimaasai eneo la Serengeti kutokana na kuzagaa taarifa kwenye mitandano ya kimataifa kuwa, muda wowote kampuni kubwa ya uwindaji itasaini mkataba utakaowaondoa katika ardhi yao ili kuwapisha Wafalme kutoka Mashariki ya Kati, walitumie eneo hilo kuwinda simba na chui.
Hata hivyo taarifa hizo, zimepingwa vikali na serikali kupitia kwa Waziri wa Maliasili na Utalii, Balozi Khamis Kagasheki, akisisitiza kuwa uvumi huo si wa kweli na hauna msingi wowote.
Taarifa zilizochapishwa kwenye mtandao wa kimataifa wa AVAAZ.org Agosti 10 mwaka huu, zinadai kuwa mpango huo utakaowaathiri Wamaasai 48,000 unaweza kuzuiliwa kabla ya kuidhinishwa na Rais Jakaya Kikwete, kama hatua zitachukuliwa sasa, kuzuia uuzwaji wa eneo hilo.
Taarifa hiyo inawataka watu kutoka duniani kote kujiorodhesha ili wafikie angalau 150,000 ili kumshinikiza Rais Kikwete kuacha kusaini mkataba ambao utafanya uhamisho huo utekelezwe.
“Kama wananchi kutoka duniani kote, tunakuomba upinge jaribio lolote la kuwahamisha Wamaasai kutoka katika ardhi yao ya kitamaduni au kuwataka waiachie kwa lengo la kuwaezesha wawindaji wa kimataifa. Tunakuhesabu kama shujaa kwa watu wako na kuzuia jaribio lolote la kubadili haki ya ardhi yao kinyume na matwaka yao,” ulisomeka ujumbe huo.
Hata hivyo, Waziri Kagasheki katika taarifa yake kwa vyombo vya habari alisema kuwa hatua kama hii haiwezi kuchukuliwa na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Hifadhi ya Serengeti maana hakuna watu wanoishi ndani ya hifadhi hiyo.
Alisema kuwa wala kitendo hicho hakijapangwa kufanyika katika Wilaya ya Serengeti iliyoko mkoani Mara, kwamba hata kama taarifa hiyo ilimaanisha Wilaya ya Serengeti mkoani Mara, bado siyo kweli maana wilaya hiyo haina idadi ya Wamasai wanaofikia jumla ya 48,000.
“Ndani ya Hifadhi ya Serengeti hakuna eneo lolote ambalo limetengwa kwa ajili ya wafalme wa Mashariki ya Kati ili waweze kulitumia kwa uwindaji wa simba na chui,” alisema.
Aliongeza kuwa, habari hizo siyo kweli maana Rais Kikwete hahusiki kabisa na ugawaji wa vitalu vya uwindaji popote pale nchini. Kwamba hiyo ni kazi ya Wizara ya Maliasili na Utalii, na wizara hiyo haijafanya hivyo katika eneo tajwa.
Waziri Kagasheki aliwaasa watu waliojiorodhesha, na wanaotarajia kujiorodhesha, kuwa wamepotoshwa, hivyo wanatakiwa wasisaini kubariki kitu mbacho hawakijui wala hakipo.
Chanzo: Tanzania Daima