Dotto Kahindi, Paris,
Ufaransa
Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) Balozi Dr. Richard Sezibira
|
Mipango ya
kimaendeleo katika nchi za Umoja wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC) inaweza
kushindwa kufanikiwa kutokana na athari za mabadiliko ya tabianchi zinazoweza
kuathiri utekelezaji wa mipango hiyo.
Katibu Mkuu wa
Umoja huo Balozi Dr. Richard Sezibira anasema kuwa kukosekana kwa sera ya
pamoja ya mabadiliko ya tabianchi itakayoainisha maeneo ya vipaumbele na namna
ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi sambamba na ukuzwaji wa viwanda ni
changamoto kubwa katika maendeleo ya nchi wanachama wa Jumuiya hiyo.
Akizungumza na
mtandao wa tabianchi (http://tabianchi.blogspot.fr/) wakati wa Mkutano
wa Kimataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi COP21, unaoendelea Paris, Ufaransa, Dr.
Sezibira anasema ili kuboresha uchumi wa Afrika Mashariki ni muhimu kuwepo kwa
sera ya mabadiliko ya tabianchi itakayokwenda sambamba na uanzishwaji wa mfuko
wa mabadiliko ya tabianchi kwa nchi z Afrika Mashariki.
Sera hiyo itatoa
vidokezo muhimu vya namna changamoto za mabadiliko ya tabianchi zinavyoweza
kutumia kama fursa za kiuchumi na kuchochea maendeleo katika ukanda huo hasa
katika sekta ya kilimo na viwanda.
Jumuiya ya Afrika
Mashariki ambayo inajumuisha nchi za Jamhuri ya Burundi, Kenya, Rwanda, Uganda
na Jamhuri ya Muungano wa Tanzania zimefanikiwa kuwasilisha mchango wake wa
kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi (Intended Nationally Determined
Contributions – INDCs). Kila nchi iliyowakilishwa katika COP21 wamewasilisha
mchango wao na kujifaragua kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa.
Pamoja na michango
hiyo kuwashirikisha wadau kutoka sekta binafsi, mashirika ya serikali ngazi za
kitaifa na wanaharakati wa mazingira, lakini hakukuwa na ushirikishwaji wa
pamoja baina ya nchi na nchi ndani ya jumuiya hiyo.
Kukosekana kwa
ushirikiano huo wa kuandaa INDC’s kunaweza kuathiri utekelezaji wa shughuli au
miradi mtambuka ya mabadiliko ya tabianchi ambayo inahitaji ushiriki wa pamoja
wa nchi wanacham wa jumuiya ili kufikia lengo.
Hata hivyo Richard
Sezibira anasema ili kuhakikisha nchi katika Jumuiya ya Afrika Mashariki
zinashirikiana pamoja katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi wameanza
taratibu za kuunda Sera na Mkakati wa Mabadiliko ya Tabianchi itakayowezesha
kupata mswaada wa mabadadiliko ya tabianchi.
“Kwa sasa
tuko kwenye majadiliano na baadae mswaada utawasilishwa kwenye bunge la
Afrika Mashariki mara baada ya kupitishwa na mawaziri wa nchi husika” anasema Dr.
Sezibira.
Kulingana na Dr.
Sezibera jambo la pili wanalolishughulikia ni kuanzishwa kwa mfuko wa
mabadiliko ya tabianchi wa Afrika Mashariki ambapo majadiliano yanaendeleo ili
kujua mfumo wa mfuko huo utakuwaje.
“Majadiliano
yanaendelea ili kujua kama mfuko huu ujitegemee au uwe ndani ya mfuko mwingine
ambao upo tayari, na mfuko huu unalenga kusaidia shuguli za kubabiliana na
mabadiliko ya tabianchi na kupunguza athari zake” anasema.
Dr Sezibera anakiri
kuwa mipango ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi inaweza kuathiri pia
shughuli za kimaendeleo katika nchi za Afrika Mashariki, hasa maendeleo ya
viwanda kwakuwa dunia ya sasa inahitaji kuwa na viwanda rafiki wa mazingira.
“Ili mipango yetu
ya maendeleo iendane sambamba na kupunguza uzalishaji wa hewa ukaa, tumeanzisha
kituo cha nishati mbadala cha Afrika Mashariki, tunahitaji kushirikiana pamoja
ili kufikia mipango hii kwa manufaa ya jumuiya yetu” anasema.
Kwa Upande wake
Mwakilishi wa Shirika la Environment Compliance Institute (ECI) nchini Kenya,
Gerry Opondo (pichani) anasema kuandaliwa kwa INDCs hakujazingatia umoja wa nchi za
Afrika Mashariki jambo linaloweza kuathiri juhudi za umoja huo za kukabiliana
na mabadiliko ya tabianchi.
“Kuna mipango
mizuri EAC ya kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi lakini mipango hiyo
inaweza kupata kigugumizi katika utekelezaji wake kwa kuwa INDC’s
zilizowasilishwa zinalenga nchi moja moja, ambazo zinaweza kupingana
katika utekelezaji wake” anasema Opondo.
Opondo anadadisi
kuwa baada ya makubalino ya Paris kufanyika, INDC’s hazitakuwa michango bali
zitageuka kuwa matakwa ya lazima ya kila nchi kuyatekeleza na ingekuwa ni jambo
jema kama mataifa yote ya EAC yatatekeleza ili kunufaisha nchi zote za jumuia
hiyo.