Uhuru na Fagio: Tusafishe mioyo yetu, Tuzibue mitaro na mifereji ya fahamu zetu, ili tuwe Huru kweli kweli

"Uhuru ni Jasho" Tumuunge mkono Mhe Rais @MagufuliJP kwa kufanya usafi tukiadhimisha siku ya Uhuru wetu. pic.twitter.com/XgoNPt... thumbnail 1 summary

Dotto Kahindi
Leo Tanzania inaazimisha miaka 54 ya Uhuru wake. Katika karne hii ya sayansi na teknolojia Uhuru wa mtu, jamii, nchi ama taifa unapaswa kuendana na Maendeleo. Bila kuwepo maendeleo ni vigumu kufanikiwa kwa uhuru huo kikamilifu.

Katika kitabu chake Mwl Nyerere cha Uhuru na Maendeleo, anasema kuwa Uhuru na Maendeleleo ni vitu vinavohusiana sana. Uhusiano wake ni kama kuku na yai, bila ya kuku hupati yai, na bila ya mayai hupati kuku, vivyo hivyo bila ya uhuru hupati maendeleo na bila ya maendeleo uhuru hautakuwepo.

Hata hivyo maendeleo ya nchi yanahitaji usafi, si usafi wa kuchukua fagio na nyenzo nyingine za kufanyia usafi ili kusafisha, kuzibua na kutindua makoko ya uchafu ambayo yamekwama katika maeneo yetu bali ni usafi wa mioyo yetu pia

Kwa kuona umuhimu wa usafi, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Dkt. John Pombe Joseph Magufuli akaamua kuwa maadhimisho ya Sherehe za Uhuru na Jamhuri tarehe 9 Desemba, 2015, yatumike  kwa kufanya kazi na usafi 

Rais Magufuli hapa uko sawa kabisa, hujakosea maana Watanzani tumejawa na roho chafu, uzembe, mifereji na mitaro ya fikra zetu imeziba, na inahitaji kuzibulia ili tuweze kufikiria sawasawa.

Mitaro ya ufisadi, rushwa, magonjwa, kukosa uwajibikaji, elimu duni, umasikini, ujinga vinahitaji siku maalumu kuviondoa, na siku hii ni 9 desemba, siku ya uhuru, tunataka tuwe huru kwelikweli. 

Ni vizuri kuitumia siku hii kutafakari na kuziondoa taka ndani ya moyo wako, nafsi yako, taka kwenye mwili wako, kazini kwako, nyumbani kwako, na zile taka ngumu za kukosa uzalendo ili sote tuifurahie Tanzania iliyosafi na salama pasi na kipindupindu.