TBN yaalaani matumizi mabaya ya kazi za wanachama wake unaofanywa na waandishi/wahariri wa magazeti na televisheni nchini

Chama cha Wamiliki/Waendeshaji wa Mitandao ya Kijamii nchini 'Tanzania Bloggers Network' (TBN) kinasikitishwa na kulaani vit... thumbnail 1 summary

Chama cha Wamiliki/Waendeshaji wa Mitandao ya Kijamii nchini 'Tanzania Bloggers Network' (TBN) kinasikitishwa na kulaani vitendo vya baadhi ya Vyombo vya Habari kutumia kazi za wanachama wake (picha, video, habari) bila idhini na bila kutoa maelezo stahiki ya vyanzo vya kazi hizo.

Taarifa iliyotolewa na Kamati ya Uongozi TBN Taifa Julai 11 mwaka huu, inaeleza masikitiko yake hayo kufuatia Gazeti la kila siku la Majira, toleo namba 8217 la Alhamisi Julai 7, 2016 ambalo bila aibu lilichukua picha katika Mtandao wa Michuzi Blog ina kuitumia pamoja na malezo yake bila ridhaa wala kutoa  kueleza chanzo cha hiyo picha. 
 
Juu ni picha inayolalamikiwa kuwa imetumiwa na gazeti la majira na chini ni picha hiyohiyo ikiwa na logo ya Michuzi blog ambaye ndiye aliyehusika kuipiga
 
Katika picha ambayo ilitumiwa na gazeti hilo, Wahariri wa Majira kwa makusudi waliondoa alama maalum ya kumbukumbu iliyowekwa katika picha hiyo (watermark-logo) na kuichapisha katika ukurasa wa mbele wa gazeti hilo, bila kutaja chanzo chake, jambo ambalo ni ukiukwaji wa Sheria na kinyume na taaluma ya habari. 
"Kitendo hicho ambacho pia kimekuwa kikifanywa na baadhi ya magazeti hapa nchini kimeonesha dhahiri ni jinsi gani baadhi ya vyombo vyenye tabia hiyo visivyothamini kazi za ‘bloggers’ na mchango wake kwenye tasnia nzima, huku wakiendelea kulea waandishi na wapiga picha wavivu na wazembe wanaotumia blogs kama njia ya mkato kupata material" inaeleza taarifa hiyo
Hata hivyo TBN kwa kutambua kuwa si vibaya vyombo vya habari kutegemeana ama kushirikiana kwa kutumia kazi za chombo kingine lakini inasisistiza kuwa ni vema chombo kinachotumia kazi ya mtu mwingine kumtambua kwa kumtaja katika kazi hiyo ama kukubaliana na chombo husika kabla ya kufanya hivyo. 
"Chama cha Wamiliki/Waendeshaji wa Mitandao ya Kijamii nchini hakitafumba macho kuona kazi za wanachama wake zikitumiwa na vyombo vingine vya habari bila utaratibu na wala makubaliano ya kabla kwa wahusika" Inaeleza zaidi taarifa hiyo